164 IZRAELI wake Mungu

164

1. Israeli wake Mungu, kimya sana, wa’zunguka Yeriko kwa imani. Malaika wake aliwaongoza, na waliendelea kwa kushinda.

Pambio:
Twende kwa kushinda, twende kwa kushinda! Kwa damu yake Yesu, twende kwa kushinda! Tegemea Mungu, anatuongoza, na kwa imani, twende kwa kushinda!

 

2. Na Daudi, mchungaji, alikwenda mbele yake Goliathi bila woga; kwa imani alitupa jiwe lake, kwa jina lake Mungu akashinda.

 

3. Danieli aliomba kila siku, hakuhofu pango la simba kamwe; katika imani aliomba Mungu, akaokoka katika hatari.

 

4. Hata safarini huku kwenda mbingu nikipita katika jangwa kavu, na kupatwa na ‘jaribu mbalimbali, najua kwa imani nitashinda.

 

5. Na imani inashinda hali zote, inaruka juu ya mambo yote. Niliye dhaifu sitahofu kamwe, kwa kuwa Mungu ananiokoa.

William Grum




165 NITAZAMAPO kwa imani

165

1. Nitazamapo kwa imani Mwokozi wangu, nafurahi, naona utajiri wake anao Mungu, Baba yangu. Haleluya! Furaha kubwa, aniongoza siku zote! Nikiuona udhaifu, anichukuwa mikononi.

 

2. Sitasumbuka mimi tena, furaha inanijaliza; Na kwa upendo na rehema anisikia, nikiomba. Haleluya! Ananitunza, Ninastarehe kwa salama. Na ukitaka raha yake, mfungulie moyo wako!

 

3. Nilipokaa kati’ dhambi Nikaliona sikitiko, Lakini shaka na hukumu Zimeondoka kwangu sasa. Haleluya! Anipa nguvu Yakuyashinda majaribu. Rohoni mwangu nina raha, Nalindwa nayo siku zote.

 

4. Dhihaka na mateso yote si kitu kwangu kwa sababu nafarijiwa na Mwokozi, nakumbatiwa na babangu. Haleluya! Mwokozi wangu ananitunza kwa neema. Nikiwa na ‘dhaifu tena, natiwa nguvu kwa imani.

Samuel Gustavsson, 1930




166 TUKIENDA pamoja

 166

1. Tukienda pamoja, tukishikamana na Mungu, tunapata amani na raha; tukifanya daima yanayompendeza, yu karibu kutusaidia.

Pambio:
Raha, furaha twazipata kwa Yesu, tukidumu katika kuamini, kutii.

 

2.Ikiwapo dhoruba, na mawimbi ya’vuma, yanakoma kwa neno la Yesu. Tukiona jaribu na kuhofu adui, tutashinda kwa nguvu ya Yesu.

 

3. Tukibeba mizigo anatustarehesha, tunapata furaha halisi. Masumbuko yatoka, giza inageuka kuwa nuru njiani mwa Mungu.

 

4. Tuna raha ya Mungu katika mashindano tukitii na tukiamini. Jua lake la pendo linawaangazia watiio na waaminio.

J.H. Sammis




167 NINAJUA Rafiki mwema

 167

1. Ninajua rafiki mwema, anitunza sana kila siku. Ayaponya majeraha na machozi ayafuta. Jina lake ni Yesu Kristo.

Pambio:
Najua rafiki mwema, na yeye ajaa ne’ma. Nikiomba asikia, afariji nikilia. Ndiye Yesu, na si mwingine.

 

2. Nimepata rafiki mwema, afariji na kunipa raha. Nikitegemea yeye sitahofu maadui; na rafiki ni Yesu Kristo.

 

3. Nifikapo mtoni pale paitwapo “kufa” na “mtego”, sitafadhaika hapo, Yesu atakuwa nami; ni rafiki mkubwa mno.

 

4. Pwani nzuri ya huko juu nifikapo kwa neema kuu, nitaimba kwa kinubi, nitasifu Yesu sana kwa upendo na urafiki.

Peter Blhorn, N. Cronsie, 1914
Oh, the best friend to have is Jesus, R.S. 88




168 NINA mshirika nafuraha kubwa

168

1. Nina ushirika na furaha kubwa, namtegemea Bwana Yesu. Wingi wa uheri kwa waaminio: Kustarehe mikononi mwake!

Pambio:
Raha, raha, raha kwa Yesu na amani! Raha, raha, nastarehe mikononi mwake.

 

2. Raha ya ajabu ni rohoni mwangu, namtegemea Bwana Yesu. Nuru huangaza njia niendayo; nastarehe mikononi mwake.

 

3. Woga na huzuni zinatoka kwangu, nikitegemea Bwana Yesu. Ninafarijiwa siku zote naye, nastarehe mikononi mwake.

E.A. Hoffman
What a fellowship, R.S. 377; R.H. 482; MA.




169 ASKARI wa imani sisi

169

1. Askari wa imani sisi, kwa shangwe tunaendelea, hata vita ‘kiwa kali tuna nguvu na ‘hodari. Tuna upanga wa imani, ni neno lake Mungu wetu; na kwa jina lake Yesu tunashangilia sasa.

Pambio:
Mbio tutaacha huku, vita ikiisha. Tutaingiamo mbingu ku starehe humo. Wao washindao huku, watapewa taji kwa mkono wa Mwokozi, anayewapenda.

 

2. Tuvae kila mtu sasa silaha zote zake Mungu. Na mishale ya shetani ‘tazimika mbele yetu. Tukimtii Bwana Yesu, twaendelea kwa ‘hodari, na kwa nguvu za ahadi tutakuwa washindaji.

 

3.Na ukipungukiwa nguvu, katika vita ukishindwa, Yesu atakutilia nguvu mpya ya kushinda. Kwa nyimbo za kushangilia, utahimili shida zote, na kupata kuokoa wenye dhambi na makosa.




170 NIKIONA shida huku katika safari

170

1. Nikiona shida huku katika safari, Yesu aninong’oneza neno la faraja. Ananipa raha tele na furaha ya ajabu. Ninaandamana naye sasa na milele.

 

2. Tena njia ikienda juu ya milima, ninakaribia mbingu, nuru inaang’aa. Na katika nuru hii ninaona kwa uwazi nchi ya ahadi yake na urithi wangu.

 

3. Kwa imani ninaimba, hata hatarini, njia ‘kiwa ndefu huku, nitavumilia. Nyota za ahadi zake zinang’aa kwa usiku, zinaniongoza vema hata huko juu.

 

4. Kama Musa aliona nchi ya ahadi, kadhalika natazama nchi yangu juu; ninaisalimu sasa hwa uheri na imani. Natamani kufikako, kwa urithi wangu.

 

5. Vya hatari vikifika kati’ njia tena, Yesu yu pamoja nami, anichunga vema. Ninaendelea mbele, na mbinguni nifikapo nyimbo nzuri nitaimba na wakristo wote.

Werner Skibsted, Paul Ongman, 1930




171 MWENYEZI Mungu ngome kuu

 171

1. Mwenyezi Mungu ngome kuu, silaha ya imara! Katika shida na huzuni twategemea yeye. Mwovu akitukaribia kututia woga, akijithibitisha kwa hila na jeuri, tusimwogope yeye!

 

2. Kwa nguvu yetu tu dhaifu, na tungeshindwa hima, ila Mwenyezi yupo nasi, twaambatana naye. Ukitaka jina lake, ndilo Yesu Kristo; aliye mshindaji na mwenye mamlaka, Mfalme wa milele.

 

3.Na dunia yote ikijaa majeshi ya giza, tuliye naye Mungu wetu, hatutaona hofu. Mwovu amehukumiwa, hana nguvu tena ya kutuangamiza maungo wala robo; ashindwa na Mwenyezi.

 

4. Maneno yake Mungu wetu, tushikamane nayo! Hatushindii vya dunia, vya juu twatafuta. Tu hodari siku zote, hata hatarini; uzima twauweka kutii Mungu wetu: Ufalme una yeye.

M. Luther, 1528
A mighty fortress is our Gud, R.H. 431




172 SISI tu viungo vya mwili’ moja

172

1. Sisi tu viungo vya mwili ‘moja, tunasaidiana. Utumishi wetu tunaupenda na twasaidiana. Twasaidiana sote, twasaidiana sote. Twamaliza kwa shangilio na kwa bidii kazi yetu.

 

2. Twafurahi kwa utumishi, hata tukiwa peke yetu; walakini heri zaidi kama tukisaidiana. 3.Ikiwezekana kwa mchwa ‘dogo kujenga kisuguu, sisi nasi kwa nguvu yake Mungu tutamaliza kazi.

 

4.Na umoja wetu ni wa thamani, unapendeza Mungu; anatubariki kwa neema, anatupa tunu kubwa.

 

5. Twakuomba, Bwana, ‘tuunganishe, tujaze pendo lako! Na kwa Roho yako utubatize, tuhudumie wewe!

A.L. Skoog, 1856-1935




173 MAISHA katika dunia

173

1. Maisha katika dunia ni kama kupanda na ‘vuna: Apandaye katika mwili atavuna uharibifu; tukitumikia Mwokozi tutapata thawabu mbinguni; yafaa kuishi na kufa katika maneno ya Mungu.

 

2. Kwa neema kubwa kabisa tumekubaliwa na Mungu, kwa neema kubwa zaidi twapata kumtumikia. Kuishi kwa ‘jili ya Yesu kati’ yote ya dunia hii na kuitangaza injili ni faida kwetu kabisa.

 

3. Wakristo wata’poingia mbinguni kusifu Mwokozi, na mimi nataka kufika kuimba pamoja na wao. Tutamshukuru Mwokozi aliyetununua kwa damu; waliohudumu kwa pendo watamhimidi milele!

 




174 PENDO kubwa la Babangu linang’aa siku zote

 174

1. Pendo kubwa la babangu linag’aa sikuzote, walakini anataka sisi tuwe nuru huku!

Pambio:
Nuru yetu iangae mbele ya wenzetu huku, hata mtu ‘moja moja aione njia njema!

 

2.Dhambi zimetia giza huku chini duniani, walakini watu wengi wanatazamia nuru.

 

3.Ndugu yangu, angalia, taa yako iwe safi! Na kwa nuru waokoe wenzi waliopotea!

P.P. Bliss
Brightly beams our Father’s mercy, R.S. 455




175 SHAMBA la Mungu limeiva

175

1. Shamba la Mungu limeiva, litayari sasa kuvunwa. Wavunaji mfike mbio kuyavuna mavuno yake!

Pambio:
Bwana Yesu, twakuomba, uwatume watenda kazi wakusanye miganda yote kwako Yesu, Mwokozi mwema!

 

2.Uwatume mapema sana, na wengine kati’ mchana, hata saa ya magharibi uwaite wavuni wako!

 

3. E’mkristo anakuita, wende mbio, usichelewe! Macho yako uyainue kwani Yesu aja upesi!

J.O. Thompson, 1894




176 MUNGU akutaka kati’ shamba lake

176

1. Mungu akutaka kati’ shamba lake, nenda na wengine kumtumikia! Ujitowe kweli kwake Mungu wetu! Uhubiri neno lake pande zote!

 

2. Ukumbuke Yesu, jinsi apendavyo! Anawatafuta waliopotea. Uwapende nawe kwa upendo wake, naye atakupa nguvu na baraka!

 

3. Uliyemwamini nenda mbio sana kati’ shamba lake, usingoje bure! Utumike vema, omba kwa bidii, na thawabu yako utaipokea!

F.R. Engelke




177 NIPE habari ya Yesu

177

1. Nipe habari ya Yesu, uiandike rohoni! Uniimbie zaburi ya kumsifu Mwokozi, sifa iliyotangazwa na malaika zamani: Mungu wa ju’ atukuzwe, iwe amani duniani!

Pambio:
Nipe habari ya Yesu, uiandike rohoni! Uniimbie zaburi ya kumsifu Mwokozi!

 

2. Nipe habari ya Yesu, jinsi alivyohimili shida, jaribu na teso na umaskini na bezo (sic)! Maradhi zangu (sic) na dhambi aka’chukuwa mwenyewe, kila wakati tayari kusaidia wahitaji.

 

3. Nipe habari ya Yesu, ya msalaba na kufa, taja kaburi mwambani, alipotoka Mwokozi! Pendo la Yesu ni kubwa, aliyekufa Golgotha, akafufuka hakika, namshukuru siku zote!

Frances J. Crosby-van Alstyne
Tell me the story of Jesus, R.S. 456; R.H. 150; MA. 206




178 YESU kutoka mbinguni aliingia huku nchi

178

1. Yesu kutoka mbinguni aliingia huku chini ya giza na dhambi, ili atuokoe.

Pambio:
Nenda, nenda! Fanya mapenzi ya Yesu! Omba kupata sehemu kati’ ya mavuno makubwa!

 

2. Wanapotea gizani wengi wa ndugu zako. Nenda kapashe habari: “Leo wokovu uko”!

 

3.Nenda kawaubirie watu wa mataifa neno la Yesu Mwokozi! Anakuita leo.

Paul Rader




179 SIKU moja mavuno yataisha kabisa

179

1. Siku moja mavuno yataisha kabisa, baada ya hayo hukumu.
Jua litazimika siku hiyo ya mwisho, na hutasikia injili

Refrain:
Atakusanya ngano kwa furaha ghalani bali makapi yote yatatupwa motoni rafiki utakuwa wapi

2. Mahubiri na nyimbo za wokovu wa mungu zitakaponyamaza huku,
uliyelikataa neno zuri la mungu, utakaa wapi milele

Refrain:
Atakusanya ngano kwa furaha ghalani bali makapi yote yatatupwa motoni rafiki utakuwa wapi

3. Watu wote wa mungu wafikapo mbinguni kukaa pamoja na yesu,
wataimba kabisa kwa sauti nguvu kumshangilia mwokozi

Refrain:
Atakusanya ngano kwa furaha ghalani bali makapi yote yatatupwa motoni rafiki utakuwa wapi


 

 




180 BWANA Yesu anatuuliza: ”Nimtume nani mavunoni?”

180

1. Bwana Yesu anatuuliza: “Nimtume nani mavunoni? Watu wenye dhambi wapotea, watolee Neno la neema! ”

Pambio:
“Mungu wangu, sema nami! Uniguze sasa kwa makaa! Mungu wangu, sema nami! Mimi hapa, unitume sasa!”

 

2. Mtumishi wake Bwana Mungu alisema: “Mimi sistahili”. Aliposikia moto safi, akasema: “Unitume mimi”!

 

3. Mataifa mengi wanakufa, hawajui Yesu na wokovu.Twende kwao mbio, tuhubiri neno la wokovu wake Yesu!

 

4. Siku za mavuno zitapita, watumishi watarudi kwao. Bwana wao atawapokea na kusema: “Ulifanya vema”!

Hear the Lord of harvest, R.H. 559





181 TUTAZAME kule mbele

181

1. Tutazame kule mbele, asubuhi inakuja! Tuamini Mungu wetu, atafanya kazi yake, kufukuza mashetani, kumiliki nchi yote. Tutashinda tukiomba, Mungu anatusikia.

 

2. Tarumbeta linalia, tuamke wote sasa! Mungu wetu anataka sisi sote tutakaswe! Kila mtu awe safi katika kanisa lake! Uliache nung’uniko, utapata nguvu yake!

 

3. Imba ninyi, watu wake, Bwana yu pamoja nasi! Tutashinda majaribu kwa uwezo wake Yesu. Twende tumhudumie kwa kumpa mali yake; hata roho na akili zimtumikie Bwana!

 

4. Watu wengi hawajui njia yakufika mbingu, wanakuwa wamefungwa kwa mikono ya shetani. Twende tukawatafute, tuwavute kwa Mwokozi, na kuomba na kukesha hata kuja kwake Yesu!




182 KISA cha kale nipe

 182

1. Kisa cha kale nipe, habari ya mbinguni, ya Bwana Mtukufu, ya pendo lake Yesu! Niambie neno lake, nipate kusikia, mnyonge mimi huku, mjinga, mkosaji. Kisa cha kale nipe, kisa cha kale nipe, kisa cha kale nipe, cha pendo lake Yesu!

 

2. Sema kwa taratibu nipate kuelewa habari ya wokovu na damu ya Mwokozi! Simulia mara nyingi, nisije kasahau, niikumbuke tena maisha yangu yote!

 

3. Taja habari hiyo kwa wema na kwa pendo, Mwokozi alikufa kutukomboa sote. Na ikiwa unataka kunifariji mimi, nisimulie ile habari ya zamani!

 

4.Nipe habari hiyo ikiwa waniona ninaipendelea fahari ya dunia! Siku nitakapo kufa ‘tapenda kusikia habari ya zamani: Mponyi mwema Yesu.

W.H. Doane
Tell me the old, old story, R.S. 132; R.H. 294




183 PANDA mbegu njema

 183

1. Panda mbegu njema, anza asubuhi, na uwaokoe watu wa shetani! Kwa wakati wake vuno litaivya, chumo utapata kwa furaha kuu.

Pambio:
:/: Twende tukavune, twende tukavune, kwa furaha kubwa twende tukavune! :/:

 

2. Panda mbegu njema juu ya milima! Na tuendelee hata mabondeni! Neno lake Mungu litawafungua watu wa gizani, kwa furaha kuu.

 

3. Panda mbegu njema hata kwa machozi, ukumbuke Yesu, leo uhubiri! Bwana wetu, Yesu, atakuja tena na thawabu yetu kwa furaha kuu.

A.M. Simpson
Sowing in the morning, R.S. 463




184 NITAKWENDA mahali pa giza

184

1. Nitakwenda mahali pa giza na dhambi kuhubiri Injili ya nuru, ili watu wasiosikia habari wafahamu upendo wa Yesu.

Pambio:
Nitakwenda mahali pa giza na dhambi, hata wote wapate kuona wokovu.

 

2. Akitaka niende kwa watu wagumu na kuacha rafiki na ndugu, hata wakinitaja: ” ‘pumbavu ” na “bure”, nachagua mapenzi ya Yesu.

 

3.Uliyezipoteza dakika na saa kwa tamaa ya mambo ya huku, uamke na uwaokoe wenzako, hata wasipotee kwa dhambi!

 

4. Watu wengi wangali watumwa gizani, wanangoja kupata uhuru, Yesu ananituma, niende upesi kuhubiri maneno ya nuru.

Margeret M. Simpson




185 NEHEMA kubwa ya Mungu wetu

185

1. Neema kubwa ya Mungu wetu: Alikutuma kwa kazi yake kwenda kuzipanda mbegu njema katika roho za wenzako!

Pambio:
Nenda, E’ mvunaji, nenda, e’mvunaji! Nenda kapande mbegu njema, nenda, e’mvunaji!

 

2. Njia ikionekana ndefu, neno la Mungu ni aminifu: “Kwa macho yangu nakuongoza, jangwani nitafanya njia”.

 

3. Ikiwa ndugu hawakuoni, mtumikie Mwokozi vema! Bwana anayetazama wewe, anampenda mwaminifu.

 

4. Hata ukiwa mdogo sana, nenda upesi shambani mwake, labda utaliokota suke lililoachwa na wenzako.

 

5. Neno na nyimbo hazitatosha kuwaamsha wafanya dhambi, bali mwenendo ulio safi utawavuta ndugu zako.

 

6. Na usichoke kupanda mbegu katika pendo na tumaini! Ukizipanda kwa shida nyingi, kwa shangwe kubwa utavuna!

 

7. Siku za kazi zita’pokwisha tutahamia mbinguni juu; tutawaona wenzetu wote tuliovuta kwa Mwokozi.

Eric Bergqvist 1898




186 FANYIA Mungu kazi

186

1. Fanyia Mungu kazi, mbio usiku waja! Mtumikie Mungu siku zako zote! Anza mapema sana, dumu mchana kutwa! Mbio usiku waja, kazi itakwisha.

 

2. Fanyia Mungu kazi kama kungali jua, usipoteze bure siku zako huku! Uyatimize yote bila kukosa neno! Mbio usiku waja, kazi itakwisha.

 

3. Fanyia Mungu kazi, saa yapita mbio! Fanya bidii sana kuokoa ndugu! Mtumikie Mungu kwa nguvu yako yote! Mbio usiku waja, kazi itakwisha.

 

T. Annie L. Coghill, 1854 M. Lowell Mason, 1864
Work for the night is coming, R.S. 429




187 TUWAVUNAJI wake Mungu

 187

1. Tu wavunaji wake Mungu, kwa neno lake tunakwenda kuvuna ngano zake Yesu alizojinunulia. Kwa shangwe tunaliingiza ghalani mwake vuno lake. Tunamsifu Yesu aliyekomboa vuno lake.

Pambio:
Twende kati’ shamba lake, Bwana a’tuita! Vuno linaivya sana, usikie mwito! Siku zetu za mavuno zinatupitia mbio. Siku zetu, siku zetu zinabaki chache.

 

2. Tu wavunaji, twende sasa tukalivune vuno lake, na kwa bidii na imani tukusanye ngano ghali! Katika pendo kubwa mno anawataka wote, Yesu, na tukiacha suke dogo ataona mara moja.

 

3. Wakati wetu ni mfupi, a’ita tena, twende mbio! Atujalize uhodari, nguvu ya kuvumilia! Usichelewe bure sasa, watenda kazi ni wachache! E’mvunaji wake Yesu, utumike kwa bidii!




188 WENGI wakasema: ‘Bado’

188

1. Wengi wakasema: “Bado”, walipoitwa na Mwokozi, lakini tena wakaona wamechelewa kuokoka.

Pambio:
Njoo mbio, njoo mbio, Yesu akuita leo! Njoo mbio, njoo mbio, usichelewe, ndugu yangu!

 

2.Nawe usemaye: “Bado”, unapoitwa naye sasa, rafiki, labda utakuta mlango umekwisha fungwa.

 

3. “Bado leo”, alisema kijana ‘moja kwa ujinga. Usiku alikufa mara, na akaenda hukumuni.

 

4. “Bado leo”, wamwambia rafiki yako bora, Yesu, Ataondoka kwa huzuni, utafanyaje bila yeye?

 

5. “Bado leo”, ukumbuke ni neno la hatari kwako! Waweza kupotea pia, kukosa kuingia mbingu.

Emil Petersson, arr.